Jumamosi 25 Julai 2026 - 15:14
Arubaini ya Imam Hussein (as), ni alama ya umoja wa Umma wa Kiislamu/ Mshikamano wa wananchi umeidhalilisha Marekani na Wazayuni

Hawza/ Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Qom amesema kuwa; Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alikuwa akiitazama Swala ya Ijumaa kuwa ni kiungo muhimu katika mlolongo wa nguvu laini (Soft Power) wa mfumo wa Kiislamu, na alisisitiza kwamba Imamu wa Ijumaa ndiye msemaji wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Saiidi, Imamu wa Ijumaa wa Qom, katika hotuba za Swala ya Ijumaa ya tarehe 2 Mordad 1405 Shamsia (July 24 2026), iliyofanyika katika Muswalla Quds mjini Qom Iran, alisema kuwa; matembezi ya Arubaini, yanayohudhuriwa na mamilioni ya Waislamu kutoka kila pembe ya dunia, ni ishara ya umoja wa Kiislamu na ni udhihirisho wa mapenzi ya kimataifa kwa Imam Hussein (as).

Imamu wa Ijumaa wa Qom aliendelea kusema kuwa; ibada hii kubwa imekuwa moja ya mikusanyiko mikubwa na yenye athari zaidi ya kidini duniani. Kwa sababu hiyo, hafla hii ya kiroho ni fursa ya kufanya upya ahadi kwa malengo na misingi ya Imam Hussein (as). Pia ni alama ya mshikamano na ya kuimarisha mahusiano ya kidini, kitamaduni na kisiasa baina ya Waislamu wa mataifa mbalimbali.

Alieleza kuwa; matembezi haya makubwa kila mwaka huonesha roho ya kupambana na ubeberu dhidi ya maadui wa Uislamu kupitia ujumbe wake wa kuunganisha Umma. Hasa mwaka huu ambapo maadui wa Uislamu, wakiongozwa na Marekani mhalifu, walifanya jinai ya kumuua shahidi Kiongozi wa Umma pamoja na wananchi wasio na hatia, hususan watoto wa Shule ya Minab. Mshikamano huu utazifuta pua chafu na najisi za Marekani pamoja na Wazayuni wanyang'anyi. Muqawama na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeazimia kuipa Marekani pigo kubwa.

Msimamizi wa Haram Tukufu ya Bibi Fatimah Ma'sumah (as), akirejelea tarehe 5 Mordad, Siku ya Swala ya Ijumaa, alisema kuwa; Swala ya kwanza ya Ijumaa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilisimamishwa mjini Tehran chini ya uongozi wa Ayatullah Taleghani. Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alikuwa Imamu wa Ijumaa wa Tehran kwa zaidi ya miongo minne, na kwa takribani miongo mitatu aliongoza mtandao wa kiroho na wenye nuru wa Maimamu wa Ijumaa nchini kote.

Ayatullah Saiidi alisema kuwa; Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alikuwa akiiona Swala ya Ijumaa kuwa ni kiungo muhimu katika mlolongo wa nguvu laini wa mfumo wa Kiislamu, na alisisitiza kwamba; Imamu wa Ijumaa ndiye msemaji wa Mapinduzi ya Kiislamu. Miongoni mwa majukumu yake makuu ni kuzalisha upya dhana za kielimu na kimaarifa, misingi ya kimapinduzi, kujibu shubuha zinazoibuka ndani na nje ya nchi kwa lugha ya kisasa, kuzifafanua kwa hoja madhubuti, na kuwahudumia watu wote kwa tabia ya baba mwenye huruma.

Aidha, akitoa nasaha kuhusu heshima na Hijabu alisema kuwa; katika uwanja huu kuna makundi mawili yanayopaswa kufanya kazi katika nyanja mbili tofauti. Kundi la kwanza ni wananchi ambao wanapaswa kutoa mawaidha ya mdomo. Wajibu huu wa kijamii ukitekelezwa ipasavyo utakuwa na athari chanya, wanaoamrisha mema na kukataza maovu wanapaswa kutumia lugha nzuri na yenye staha; kwa kufanya hivyo, si tu kwamba mawaidha yao yatakuwa na athari bali pia yatawafanya watu wavutiwe na maadili mema.

Khatibu wa Ijumaa wa Qom aliendelea kusema kuwa; ikiwa mawaidha ya mdomo yatatolewa kwa lugha isiyofaa, hayatakuwa na athari yoyote, bali yanaweza kumfanya anayeelezwa awe mkaidi na wakati mwingine kusababisha ugomvi. Barabarani na sehemu za umma si mahali panapofaa kwa mijadala na ufafanuzi wa kina. Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alisema: "Jukumu letu ni kusema na kuondoka." Mwenye kuamrisha mema na kukataza maovu anapaswa kuonesha kuwa lengo lake si kumdhalilisha wala kumharibu mwenzake, bali mawaidha yake yanapaswa kuwa ya kheri na yenye nia njema.

Alisema kuwa kundi la pili ni vyombo vya mahakama na polisi ambavyo vinapaswa kuwachukulia hatua kali wanaovunja maadili ya jamii. Maafisa husika wameonya kuwa Qom ni mji wenye utambulisho wa kimapinduzi na kidini, na hakuna anayepaswa kuvuruga utulivu wa kisaikolojia wa wananchi. Wanaovunja maadili watashughulikiwa kwa ukali.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha